WAKALA wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na wataalam wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wamepongeza uwekezaji wa Tanzania katika huduma ya saratani. Ujumbe huo ukiongozwa na Dk Alfred Karagu, Mratibu wa Mpango wa Mapitio ya IAEA wiki hii ulifanya ziara katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) mjini Dodoma wiki hii na kufurahishwa na Kituo cha kisasa cha Mafunzo na Tiba ya Saratani kinachoendelea kujengwa BMH, ambacho wanaamini kitabadilisha upatikanaji wa huduma za saratani nchini. "Ziara hii, chini ya mradi wa IMPACT, imetuwezesha kutathmini uwezo wa Tanzania katika kukabiliana na saratani. Tumefurahishwa na miundombinu ya kisasa inayojengwa hapa, ambayo itakuza huduma za tiba ya mionzi na kuimarisha huduma ya saratani nchini kote," Dk Karagu alisema. Aliongeza kuwa mapitio ya aina hiyo ya mwaka 2006 yalifungua njia kwa Mkakati wa kwanza wa Kitaifa wa Kudhibiti Saratani nchini Tanzania, uliodumu hadi 2022, akisisitiza kuwa tathmini ya sasa ndiyo itakayoongoza utayarishaji wa mkakati mpya. Profesa Hanan Gewefel, mtaalam wa radiolojia na dawa za nyuklia kutoka IAEA, alisisitiza umuhimu wa uhamasishaji wa umma na uchunguzi wa kawaida, haswa kwa saratani ya matiti.
Alisifu vifaa vya hali ya juu vya BMH, ambavyo hutambua ugonjwa huo katika hatua za awali, kupunguza gharama na kuboresha maisha. Mratibu wa Kitaifa wa Saratani kutoka Wizara ya Afya, Dk Caroline Mrema, alisema hii ni tathmini ya pili ya IAEA–WHO nchini Tanzania, ya kwanza ikiwa mwaka 2006. "Mapitio ya awali yalisaidia kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Saratani, ambao ulikamilika mwaka wa 2022. Tathmini hii itaongoza uundaji wa mkakati mpya kwa ushirikiano na washikadau," alifafanua. Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abel Makubi, alisema hospitali hiyo tayari inatoa huduma ya chemotherapy na palliative, na maandalizi ya matibabu ya mionzi na nyuklia yanaendelea mara baada ya kituo hicho kukamilika. "Serikali imewekeza zaidi ya 30bn/- katika mradi huu, ambao utahudumia sio Tanzania tu bali hata nchi jirani," alisema, akiomba msaada zaidi katika vifaa na mafunzo.
