Mkazi wa Arusha atoa msaada wa 50m/- kwa mgombea urais wa CCM
ARUSHA: KIONGOZI wa Kanisa la Ngurumo ya Upako lenye makao makuu yake Mkoani Arusha, Nabii Dk.Geo Davie, ametoa msaada wa shilingi milioni 50 kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha kwa ajili ya kumuunga mkono mgombea urais wa chama hicho, Dk.Samia Suluhu Hassan.
Dk Samia anatarajiwa kufanya mikutano ya kampeni mkoani humo Oktoba mwaka huu. Nabii Geo Davie amekabidhi msaada huo siku ya Alhamisi Septemba 25, 2025 katika ukumbi wa Makao Makuu ya CCM Mkoa wa Arusha.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, alieleza kujivunia kukiunga mkono chama chake na kumtakia heri Dk Samia wakati akijiandaa na uchaguzi ujao.
"Nashukuru kupata nafasi ya kuchangia Chama chetu, Chama Cha Mapinduzi, hasa tunapojiandaa kumkaribisha Mwenyekiti wetu wa Taifa Mkoa wa Arusha katika kipindi hiki kigumu cha uchaguzi," alisema Dk. Geo Davie.
Kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha Ndugu Musa Matoroka amemshukuru Mtume Geo Davie kwa mchango wake mkubwa na wa kujitolea. Alisisitiza kuwa chama na serikali vinathamini uongozi wa kiroho wa Nabii Davie na kuendelea kuunga mkono mipango ya maendeleo ya jamii katika Mkoa wa Arusha.