Tanzania yathibitisha msimamo wake wa kuendeleza amani kupitia diplomasia
NEW YORK: TANZANIA imethibitisha dhamira yake ya kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuendeleza amani na kutatua migogoro kwa njia za kidiplomasia. Hayo yamesemwa leo Septemba 25, 2025 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabiti Kombo, aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa 1303 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika uliofanyika New York, Marekani.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Kombo alithibitisha dhamira ya Tanzania kuendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo katika kuendeleza amani na kutatua migogoro kwa njia za kidiplomasia.
Alibainisha kuwa viongozi wengi wa Afrika wanatambua hatua iliyofikiwa katika kuimarisha miundombinu ya amani na usalama katika bara zima kupitia utekelezaji wa Usanifu wa Amani na Usalama wa Afrika (APSA) na Usanifu wa Utawala wa Afrika (AGA).
"Mafanikio haya yamewezesha kuundwa kwa majukwaa ya kubadilishana ujuzi kati ya Nchi Wanachama wa AU, na hivyo kukuza mshikamano na dhamira ya pamoja katika kufikia amani ya kudumu barani Afrika," alisema Waziri Kombo.
Alikumbuka kuwa wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Umoja wa Afrika mwaka 2013, bara hilo liliweka lengo kubwa la kumaliza vita vyote ifikapo 2020 kupitia mpango wa Kunyamazisha Bunduki.
Hata hivyo, aliongeza kuwa makataa hayo yameongezwa hadi 2030 ili kuyapa mataifa ya Afrika fursa mpya ya kufikia azma ya pamoja ya amani ya kudumu katika kanda nzima.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama la AU, Rais João Lourenço wa Angola, alizitaka nchi wanachama kuimarisha juhudi za kuzuia na kutatua migogoro barani humo ili kulinda usalama na maendeleo ya watu wa Afrika.
"Ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa sasa, migogoro hii itaendelea kuhatarisha amani na utulivu wa bara hilo na kuzuia utekelezaji wa maazimio na mikataba ya AU chini ya Ajenda 2063, pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa," alisisitiza Rais Lourenço.