Tanzania inataka kugeuza Dodoma kuwa kitovu cha utalii cha ukanda wa kati

SALUM
By -
0


 DODOMA: SERIKALI ya Tanzania imeanza kutekeleza mkakati kabambe wa kuboresha vivutio vya utalii vilivyopo Dodoma na Kanda ya kati ili vivutie watalii wa ndani na nje ya nchi. Mkakati huo unalenga kuimarisha miundombinu na huduma katika maeneo ya Mkungunero, Hifadhi ya Swaga Swaga, na picha za kale za Kondoa Irangi, ambapo Wizara ya Maliasili na Utalii inashirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na wadau binafsi. KAIMU Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utalii, Dainess Kunzugala, alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha vivutio hivyo vinakuwa na barabara nzuri, hoteli za kisasa kuanzia nyota tatu, huduma muhimu za kijamii, pamoja na bidhaa na shughuli mbalimbali za kitalii. Mkurugenzi wa Epic Adventures, Joel Massai, alisema sekta binafsi imejipanga kushirikiana na serikali kutangaza na kuboresha vivutio vya Dodoma.

"Nasisitiza kuwa Mkoa wa Dodoma umebarikiwa kuwa na vivutio vya kipekee vinavyoweza kuufanya kuwa kitovu cha utalii kwa ukanda wa kati," alifafanua. Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa TFS Kanda ya Kati, Mathew Kiondo, alisema baadhi ya vivutio vikubwa vya Dodoma viko katika mapori ya akiba yanayosimamiwa na TFS, ambayo yanaendelezwa na kulindwa ili kuchochea utalii wa ikolojia. PIA SOMA: Tanzania inathamini ushiriki wa wanawake katika mnyororo wa uchimbaji madini Ofisa Utalii Mwandamizi wa TTB Kanda ya Kati, George Mwagane, alisema miradi mikubwa ya kitaifa, ikiwamo ya SGR na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, itakuwa chachu ya kukuza utalii mkoani humo. Meneja wa Kituo cha Kondoa Irangi, Zuberi Mabie, alisema idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka 1,287 mwaka 2018 hadi 7,654 mwaka 2024. “Watalii wa kimataifa wanaongezeka kutoka 171 mwaka 2020 hadi 541 mwaka 2024, kutokana na uwekezaji wa serikali katika miundombinu na huduma bora. Siku ya Utalii Duniani iliadhimishwa Septemba 27 chini ya kaulimbiu “Utalii na Maendeleo Endelevu”, ambapo zaidi ya washiriki 40 walishiriki katika ziara ya siku mbili katika kituo cha kihistoria cha Kolo, Kondoa.

Tags:

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default