Tanzania yapata mafanikio makubwa katika uchimbaji madini, uongezaji thamani madini
By -
September 29, 2025
0
GEITA: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, amesema ukuaji wa shughuli za uongezaji thamani madini nchini umechangia ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme. Akizungumza wakati wa kufunga Maonesho ya 8 ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita, alisema Serikali inaendelea kusambaza umeme kwenye maeneo ya migodi pamoja na viwanda vya uchenjuaji na uongezaji thamani madini ili kuhakikisha uzalishaji haukatiki na kuboresha ufanisi. Akifafanua Dk Biteko alibainisha kuwa ukuaji wa sekta ya madini unakwenda sambamba na ongezeko la mahitaji ya umeme nchini huku akitolea mfano kuwa mkoani Geita kwa sasa zaidi ya megawati 30 zinatumika tofauti na siku za nyuma. Aidha, alieleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha umeme unaendelea kuwafikia migodini, wachimbaji wadogo, na viwanda vya uongezaji thamani, ili sekta hiyo iendelee kukua kwa kasi na kuongeza ajira. PIA SOMA: Tarumbeta za GST kwa misalaba yake; ni bora kwa kuyeyusha sampuli za dhahabu Aidha alisema sekta ya madini imeendelea kuwa imara katika kipindi cha miaka minne iliyopita na sasa imejiimarisha kuwa moja ya nguzo muhimu za uchumi wa taifa. Awali, wakati Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikitembelea mabanda ya maonyesho, ilibaini kuwa tayari imenunua zaidi ya tani 10 za dhahabu zenye thamani ya 2.5tri/- ikiwa ni mkakati wake wa kuimarisha hifadhi za Taifa na kuepusha uchumi na majanga ya kimataifa.
Tags:
