Waziri Mkuu amtetea Dk Samia muhula mwingine wa miaka 5

SALUM
By -
0


 PEMBA: Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Dk Samia Suluhu Hassan ameendelea kujidhihirisha kuwa yeye ni mama wa maendeleo kwa kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kijamii na kiuchumi nchini. Akiwahutubia wananchi wa Jimbo la Kojani Pemba, Majaliwa alisema Serikali ya Awamu ya Sita imefanikisha ujenzi wa vituo vya afya vyenye uwezo wa kutoa huduma zote za msingi jambo ambalo limepunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kupata huduma hizo. "Kwa sasa, wananchi hawatakiwi kusafiri umbali mrefu kupata huduma za afya, wataalamu wa afya wameajiriwa," alisema. Alibainisha kuwa Rais Dk.Samia pia ametekeleza maono yake ya kupiga ndoo kichwani kupitia utekelezaji wa miradi ya maji mikubwa, ya kati na midogo, sambamba na kuvutia wawekezaji waliowekeza kwenye miradi mikubwa ambayo imetoa ajira kwa Watanzania. PIA SOMA: CCM yawahakikishia wakazi wa Moshi ari ya kuwainua wananchi kiuchumi Majaliwa alisisitiza kuwa Rais Samia ndiye mgombea pekee mwenye dira ya kuibadilisha Tanzania, huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Oktoba 29. Katika mikutano hiyo, Majaliwa alimpongeza mgombea Urais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi, kwa kuifungua Zanzibar kiuchumi na kugusa sekta mbalimbali za kijamii. “Uongozi wa Dk. Mwinyi umegusa kila sekta ikiwa ni pamoja na miundombinu, elimu, afya, maji, michezo na huduma nyinginezo, yeye ni Daktari wa Maendeleo, nendeni mmpigie kura,” alisema. Aidha, Majaliwa alimtaka Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kojani, Hamad Chande, akimtaja kuwa ni mtendaji, mzalendo na mchapakazi. "Namfahamu Chande ndiyo maana aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha, mchagueni ili aendelee kuwaletea maendeleo," alisema. Kwa upande wake Chande aliwaomba wananchi wa Jimbo hilo kumpa ridhaa ya kuendelea kuwa mbunge wao huku akiahidi kusimamia kikamilifu shughuli za maendeleo.

Tags:

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)
3/related/default